9. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu.
10. Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele.
11. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
12. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.
13. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.