18. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?
19. Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?
20. Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.
21. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.
22. Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?
23. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.
24. Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.
25. Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;
26. maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.
27. Na mtu asiyeamini akiwaalika, nanyi mnataka kwenda, kuleni kila kitu kiwekwacho mbele yenu bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri.
28. Lakini mtu akiwaambia, Kitu hiki kimetolewa kiwe sadaka, msile, kwa ajili yake yeye aliyeonyesha, na kwa ajili ya dhamiri.
29. Nasema, dhamiri, lakini si yako, bali ya yule mwingine. Maana kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?
30. Ikiwa mimi natumia sehemu yangu kwa shukrani, kwa nini nitukanwe, kwa ajili ya kitu nikishukuriacho?
31. Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.
32. Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala kanisa la Mungu,
33. vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa. a.