11. hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.
12. Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.
13. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.
14. Mfalme akageuza uso wake, akawabariki mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
15. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena na Daudi baba yangu kwa kinywa chake akalitimiza kwa mkono wake, akasema,
16. Tokea siku ile nilipowatoa watu wangu Israeli katika Misri, sikuchagua mji wo wote katika kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe hapo; lakini nalimchagua Daudi awe juu ya watu wangu Israeli.
17. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
18. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.
19. Lakini wewe hutanijengea nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
20. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
21. Na humo sanduku hili nimelifanyizia mahali, ambalo ndani yake mna maagano ya BWANA, aliyoyafanya na baba zetu, hapo alipowatoa katika nchi ya Misri.
22. Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni.
23. Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.
24. Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
25. Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.