1 Fal. 7:27-37 Swahili Union Version (SUV)

27. Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.

28. Na kazi ya matako ndiyo hii; yalikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio;

29. na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng’ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na tako; na chini ya simba na ng’ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza.

30. Kila tako lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni.

31. Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya tako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana.

32. Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya tako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu.

33. Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu.

34. Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za tako moja; mataruma hayo ni kitu kimoja na tako lenyewe.

35. Na juu ya tako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya tako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo.

36. Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote.

37. Hivyo akayafanya yale matako kumi; yote yalikuwa ya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja.

1 Fal. 7