12. Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.
13. Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi BWANA.
14. Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, BWANA asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.
15. Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16. Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.
17. Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.
18. Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.
19. Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.
20. Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.
21. Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.
22. Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
23. Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.
24. Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.
25. Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.
26. Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.
27. Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.
28. Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, BWANA ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi BWANA.
29. Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.
30. Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.