18. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa;
19. kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa BWANA, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli.
20. Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
21. Ndipo watu wa Israeli wakatengwa sehemu mbili; nusu ya watu wakamfuata Tibni mwana wa Ginathi, ili wamfanye mfalme; nusu wakamfuata Omri.
22. Lakini hao watu waliomfuata Omri wakawashinda watu waliomfuata Tibni mwana wa Ginathi; basi akafa Tibni, akatawala Omri.
23. Katika mwaka wa thelathini na moja wa Asa, mfalme wa Yuda, Omri alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi na miwili. Akatawala huko Tirza miaka sita.
24. Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kuliandama jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima.
25. Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia;
26. kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.