10. tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia.
11. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo.
12. Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa.
13. Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa BWANA, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu.
14. Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa?
15. Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang’oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng’ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha BWANA.
16. Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli.
17. Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa.
18. Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii.