1. Neno la Mwenyezi-Mungu kuhusu Israeli. Mwenyezi-Mungu aliyezitandaza mbingu, aliyeiweka misingi ya dunia na kumpa mwanadamu uhai asema hivi:
2. “Nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama kikombe cha divai; na mataifa yaliyo kandokando yake yatakunywa na kuyumbayumba kama walevi. Mji wa Yerusalemu utakaposhambuliwa, hata miji yote ya Yuda itashambuliwa.
3. Siku hiyo nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama jiwe zito kwa watu wote: Yeyote atakayelinyanyua atajiumiza mwenyewe. Watu wa mataifa yote duniani wataushambulia mji huo.
4. Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitamtia hofu kila farasi, na mpandafarasi wake nitamfanya kuwa mwendawazimu. Farasi wa mataifa mengine nitawapofusha. Lakini kabila la Yuda nitalilinda.
5. Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’.