16. Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’”
17. Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’”
18. Katika maono mengine, niliona pembe nne.
19. Nami nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Pembe hizi zinamaanisha nini?” Yeye akanijibu, “Pembe hizi zinamaanisha yale mataifa ambayo yaliwatawanya watu wa Yuda, Israeli na Yerusalemu.”