Yoshua 8:17-22 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai, waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli.

18. Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai.

19. Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto.

20. Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia.

21. Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua.

22. Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao.

Yoshua 8