15. Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’”
16. Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa.
17. Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa.
18. Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa.
19. Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.”
20. Akani akamjibu; “Ni kweli nimetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Na hivi ndivyo nilivyofanya:
21. Nilipoona vazi moja zuri kutoka Shinari kati ya nyara, shekeli 200 za fedha na mchi wa dhahabu wenye uzito wa shekeli 50, nikavitamani na kuvichukua; nimevificha ardhini ndani ya hema langu; na fedha iko chini ya vitu hivyo.”
22. Basi, Yoshua akawatuma wajumbe, nao wakakimbia hemani kwa Akani. Na kumbe, vilikuwa vimefichwa hemani na fedha ikiwa chini yake.