8. Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona.
9. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali mpaka hivi leo.
10. Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko.
11. Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile.
12. Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
13. Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?”