Yoshua 22:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Walipofika kwenye mto Yordani wakiwa bado katika nchi ya Kanaani, wakajenga madhabahu kubwa sana karibu na mto huo.

11. Basi, habari zikawafikia watu wa makabila mengine ya Israeli kwamba makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase yalikuwa yamejenga madhabahu kubwa karibu na mto Yordani katika nchi ya Kanaani, yaani ndani ya eneo lao.

12. Waliposikia hivyo, Waisraeli walikusanyika wote huko Shilo kwenda kupigana vita na hayo makabila ya mashariki.

13. Basi, watu wa Israeli wakamtuma Finehasi, mwanawe kuhani Eleazari, huko Gileadi kwa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase.

14. Finehasi akaondoka pamoja na wakuu kumi, kila mmoja akiwa mkuu wa jamaa katika kabila lake.

15. Nao wakawaendea watu wa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase huko Gileadi wakawaambia,

16. “Jumuiya nzima ya Mwenyezi-Mungu inauliza hivi: ‘Ni udanganyifu gani huu mmemfanyia Mungu wa Israeli? Mbona mmemwasi Mwenyezi-Mungu kwa kujenga madhabahu hii?

17. Je, dhambi tulizotenda huko Peori hazitoshi? Hamwoni kwamba bado hatujajitakasa na kwamba mateso yake bado yanaisumbua jumuiya ya Mwenyezi-Mungu?

18. Kwa nini, basi, mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu? Mkimwasi Mwenyezi-Mungu leo, kesho ataikasirikia sana jumuiya nzima ya Israeli.

19. Haya, ikiwa nchi yenu si najisi, njoni katika nchi ya Mwenyezi-Mungu ambako hema yake iko na kujichukulia sehemu huko pamoja nasi; ila tu msimwasi Mwenyezi-Mungu na kutufanya sisi sote waasi kwa kujijengea nyinyi wenyewe madhabahu isiyo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.

20. Je, Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu katika vitu vitakatifu, ghadhabu haikuangukia jumuiya nzima ya Israeli? Tena Akani hakufa tu yeye peke yake kwa sababu ya uovu wake.’”

Yoshua 22