15. Kisha Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote.
16. Wale wafalme watano walikimbia na kujificha katika pango la Makeda.
17. Yoshua akapata habari kwamba wafalme hao wamegunduliwa walikojificha katika pango la Makeda.
18. Yoshua akasema, “Vingirisheni mawe makubwa mlangoni mwa pango na kuweka walinzi hapo.
19. Lakini nyinyi msikae huko, bali muwafuatie adui zenu. Muwapige kutoka upande wa nyuma, wala musiwaache waingie mijini mwao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.”
20. Yoshua pamoja na Waisraeli waliwapiga na kuwaangamiza wote, na wachache wao walionusurika walikimbilia kwenye miji yao yenye ngome.
21. Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli.
22. Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.”
23. Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni.