26. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake, “Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao.”
27. Halafu akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, huyo ndiye mama yako.” Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
28. Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.”
29. Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni.
30. Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho.
31. Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe.
32. Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu.
33. Lakini walipomfikia Yesu, waliona kwamba alikwisha kufa, kwa hivyo hawakumvunja miguu.
34. Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. (
35. Naye aliyeona tukio hilo ameshuhudia ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli).