1. Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko.
2. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau.
3. Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: “Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!” Wakampiga makofi.
4. Pilato akatoka nje tena, akawaambia, “Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake.”
5. Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo.”
6. Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaza sauti: “Msulubishe! Msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mchukueni basi, nyinyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake.”
7. Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kufuatana na sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.”
8. Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa.
9. Basi, akaingia ndani ya ikulu tena, akamwuliza Yesu, “Umetoka wapi wewe?” Lakini Yesu hakumjibu neno.
10. Hivyo Pilato akamwambia, “Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?”