Yohane 17:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, “Baba, ile saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza.

2. Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uhai wa milele wote hao uliompa.

3. Na uhai wa milele ndio huu: Kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma.

4. Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa niifanye.

5. Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu.

6. “Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako.

7. Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako.

8. Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa, nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma.

9. “Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea wale ulionipa, maana ni wako.

10. Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana katika hao ulionipa.

11. Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja.

12. Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule mwana mpotevu, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia.

13. Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu.

14. Mimi nimewapa ujumbe wako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.

15. Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu.

16. Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.

Yohane 17