Yohane 1:32-42 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.

33. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’

34. Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”

35. Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.

36. Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu.”

37. Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.

38. Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi, (yaani Mwalimu), unakaa wapi?”

39. Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.

40. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.

41. Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo).

42. Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Kigiriki ni Petro, yaani, “Mwamba”).

Yohane 1