Yeremia 41:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania, pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye, waliwaua watu hao na kuzitupa maiti zao kisimani.

8. Lakini palikuwa na watu kumi katika kundi hilo waliomwambia Ishmaeli: “Tafadhali usituue, maana tuna akiba kubwa ya ngano, shayiri, mafuta na asali ambayo tumeificha mashambani.” Basi hao akawaacha hai.

9. Kisima ambamo Ishmaeli alitupa maiti za wale watu aliowaua kilikuwa ni kile kikubwa, ambacho mfalme Asa alikuwa amekichimba ili kujihami dhidi ya Baasha, mfalme wa Waisraeli. Ishmaeli mwana wa Nethania, alikijaza kisima hicho maiti za wale watu aliowaua.

10. Kisha, Ishmaeli aliwateka binti zake mfalme na watu wote waliosalia Mizpa, watu ambao Nebuzaradani, kapteni wa walinzi, alikuwa amemkabidhi Gedalia mwana wa Ahikamu. Ishmaeli mwana wa Nethania, aliwachukua mateka hao, akaondoka, akaenda kwa Waamoni.

11. Lakini Yohanani mwana wa Karea, pamoja na viongozi wote wa majeshi, waliposikia juu ya uovu ambao Ishmaeli mwana wa Nethania, alikuwa ameufanya,

12. waliwakusanya watu wao wote, wakaenda kupigana na Ishmaeli. Walimkuta penye bwawa kuu lililoko Gibeoni.

13. Watu wote waliotekwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea, pamoja na viongozi wote wa majeshi, walifurahi sana.

14. Basi, watu hao wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka kutoka Mizpa, waligeuka, wakarudi nyuma, wakamwendea Yohanani mwana wa Karea.

15. Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania, pamoja na watu wanane waliponyoka kutoka kwa Yohanani, wakakimbilia kwa Waamoni.

16. Kisha, Yohanani mwana wa Karea pamoja na viongozi wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, waliwachukua watu wote waliosalia, ambao Ishmaeli mwana wa Nethania, alikuwa amewachukua mateka kutoka Mizpa baada ya kumwua Gedalia mwana wa Ahikamu, yaani: Askari, wanawake, watoto na matowashi. Yohanani aliwarudisha wote kutoka Gibeoni.

Yeremia 41