7. Shughulikieni ustawi wa mji ambamo nimewahamishia. Niombeni kwa ajili ya mji huo, maana katika ustawi wake nyinyi mtastawi.
8. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Msikubali kudanganywa na manabii wenu na waaguzi waliomo miongoni mwenu, wala msisikilize ndoto wanazoota.
9. Maana wanawatabiria uongo kwa kutumia jina langu. Mimi sikuwatuma. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’
10. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka sabini huko Babuloni, baada ya muda huo, nitawajia na kuitimiza ahadi yangu ya kuwarudisha mahali hapa.
11. Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye.
12. Hapo ndipo mtakaponiita na kuniomba, nami nitawasikiliza.