26. Kisha, kwenye kile kikapu cha mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu akatoa mkate mmoja usiotiwa chachu, mkate mmoja wenye mafuta na mkate mmoja mdogo, akaviweka vyote juu ya vipande vya mafuta na ule mguu.
27. Mose akaviweka mikononi mwao Aroni na wanawe, nao wakafanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu.
28. Kisha Mose akavichukua vitu hivyo vyote kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa. Hii ni sadaka ya kuwekwa wakfu, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu; ni sadaka itolewayo kwa moto.
29. Kisha Mose akachukua kile kidari na kufanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Sehemu hiyo ya yule kondoo dume wa kuweka wakfu ni mali yake Mose kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.