Walawi 5:7-11 Biblia Habari Njema (BHN)

7. “Lakini kama hawezi kutoa mwanakondoo wa sadaka ya kuondoa hatia kwa ajili ya dhambi aliyotenda, basi atamletea Mwenyezi-Mungu hua wawili au makinda mawili ya njiwa: Mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.

8. Atawaleta kwa kuhani, naye kuhani atamtoa mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi kwa kumkongonyoa shingo yake bila kukichopoa kichwa chake.

9. Sehemu ya damu yake ataipaka pembeni mwa madhabahu na ile nyingine ataimimina chini kwenye tako la madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi.

10. Kisha atamtoa yule wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa kulingana na maagizo. Kuhani atamfanyia huyo mtu upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.

11. “Ikiwa hawezi kutoa hua wawili au makinda mawili ya njiwa kama sadaka yake ya kuondoa dhambi aliyotenda, basi, ataleta unga kilo moja. Lakini hatautia mafuta wala ubani kwani ni sadaka ya kuondoa dhambi.

Walawi 5