Walawi 27:3-14 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Mwanamume wa miaka ishirini hadi miaka sitini atakombolewa kwa fedha shekeli 50 kulingana na kipimo cha mahali patakatifu.

4. Kama ni mwanamke, atakombolewa kwa fedha shekeli 30.

5. Kama mtu huyo ni wa miaka kati ya mitano na 20 atakombolewa kwa fedha shekeli 20 kama ni mvulana na shekeli 10 za fedha kama ni msichana.

6. Ikiwa ni mtoto wa umri wa kati ya mwezi mmoja na miaka mitano atakombolewa kwa shekeli 5 za fedha kama ni mvulana na shekeli 3 za fedha kama ni msichana.

7. Ikiwa mtu huyo umri wake ni zaidi ya miaka sitini, thamani yake itakuwa ni shekeli 15 za fedha kama ni mwanamume na shekeli 10 za fedha kama ni mwanamke.

8. Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini na hawezi kulipa gharama yake, basi, mtu huyo atapelekwa kwa kuhani. Kuhani atampima thamani yake kulingana na uwezo wa huyo aliyeweka nadhiri.

9. “Ikiwa nadhiri yenyewe inahusu mnyama wa namna ambayo watu humtolea Mwenyezi-Mungu sadaka, basi mnyama huyo huwa kitu kitakatifu.

10. Hairuhusiwi kumbadilisha mnyama huyo kwa mwingine awaye yeyote, mzuri kwa mbaya au mbaya kwa mzuri. Kama akimbadilisha kwa mnyama mwingine, wote wawili watakuwa watakatifu.

11. “Kama nadhiri hiyo yahusu mnyama najisi, wa aina ambayo si halali kumtolea Mwenyezi-Mungu, basi, mtu aliyemtoa, atamleta kwa kuhani,

12. naye kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua kuhani, ndivyo itakavyokuwa.

13. Lakini ikiwa mwenyewe anataka kumkomboa, basi, ataongeza asilimia ishirini ya thamani ya mnyama huyo.

14. “Mtu akiiweka wakfu nyumba yake kuwa takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, kuhani ataamua thamani yake kulingana na uzuri au ubaya wake. Jinsi atakavyoamua, ndivyo itakavyokuwa.

Walawi 27