8. Kila siku ya Sabato Aroni ataipanga sawasawa katika safu mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwa niaba ya watu wa Israeli kama agano la milele.
9. Aroni na wazawa wake peke yao ndio wanaoruhusiwa kula mikate hiyo kwani ni mitakatifu kabisa kwa sababu ni sehemu ya sadaka ninazotolewa mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni haki yao milele.”
10. Siku moja kukatokea mzozo huko kambini kati ya Mwisraeli mmoja na kijana mmoja wa mama Mwisraeli aitwaye Shelomithi lakini baba Mmisri.
11. Siku moja yule kijana ambaye mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri wa kabila la Dani, alilikufuru na kulilaani jina la Mungu. Basi watu walimpeleka kijana kwa Mose,
12. wakamtia ndani mpaka hapo watakapofunuliwa matakwa ya Mwenyezi-Mungu.
13. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
14. “Mtoe kijana aliyekufuru nje ya kambi, na wale wote waliomsikia akikufuru waweke mikono yao juu ya kichwa chake, na jumuiya yote imuue kwa kumpiga mawe.
15. Nawe uwaambie Waisraeli kwamba mtu yeyote atakayemlaani Mungu wake ni lazima awajibike kwa dhambi yake.
16. Mtu yeyote awe ni mwenyeji au mgeni anayemkufuru Mwenyezi-Mungu, jumuiya nzima itamuua kwa kumpiga mawe.
17. Mtu yeyote anayeua mtu mwingine ni lazima naye auawe.
18. Mtu yeyote anayeua mnyama ni lazima atoe fidia: Uhai kwa uhai.
19. Mtu yeyote anayemwumiza jirani, ni lazima naye aumizwe kulingana na kiasi alichomwumiza jirani yake,
20. amemvunja mfupa naye atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kila mtu anayemwumiza mwenzake ni lazima naye aumizwe kulingana na tendo lake.
21. Anayemuua mnyama ni lazima atoe fidia; lakini mtu yeyote akimuua mtu mwingine ni lazima naye auawe.
22. Sheria hii yamhusu mgeni na mwenyeji. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”