Walawi 23:21-30 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Siku hiyohiyo mtatoa ilani ya mkutano mtakatifu; msifanye kazi. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu.

22. “Unapovuna mavuno yako shambani, kamwe usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba lako wala usirudi nyuma kukusanya masalio. Utawaachia hayo maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

23. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

24. “Waambie watu wa Israeli hivi: Siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtaadhimisha siku ya mapumziko rasmi, siku ya ukumbusho itakayotangazwa kwa mlio wa tarumbeta na kufanya mkutano mtakatifu.

25. Msifanye kazi siku hiyo na ni lazima mnitolee mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto.”

26. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

27. “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni siku ya upatanisho. Siku hiyo ni siku ya kuwa na mkutano mtakatifu. Mtafunga na kutoa sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.

28. Msifanye kazi zenu zozote za kawaida siku hiyo. Siku hiyo ni siku ya upatanisho, siku ya kuwafanyieni upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

29. Mtu yeyote asiyefunga siku hiyo ni lazima atengwe mbali na watu wake.

30. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo nitamwangamiza miongoni mwa watu wake.

Walawi 23