11. Kuhani atafanya nayo ishara ya kunitolea siku inayofuata siku ya Sabato ili mpate kukubaliwa.
12. Siku hiyo mnapofanya ishara ya kutoa huo mganda mbele yangu mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya mwanakondoo dume wa mwaka mmoja asiye na dosari.
13. Pamoja na sadaka hiyo, mtatoa sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta ambayo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto, na harufu yake itanipendeza. Sadaka yake ya kinywaji ni lita moja ya divai.
14. Kabla ya siku hiyo ya kuniletea mimi Mungu wenu sadaka hiyo, hamruhusiwi kula mazao ya kwanza ya mavuno yenu, yawe mabichi, yamekaangwa au yemeokwa kuwa mikate. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu mahali popote mtakapoishi.
15. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku ile inayofuata Sabato ile ambapo mtaleta mganda wa sadaka ya kunitolea kwa ishara mimi Mwenyezi-Mungu.
16. Mnamo siku ya hamsini, siku ya pili ya Sabato ya saba, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka mpya.
17. Kila jamaa italeta mikate miwili ya sadaka ya kutoa kwa ishara mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Kila mkate ni lazima uwe umetengenezwa kwa kilo mbili za unga laini uliotiwa chachu; na huo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu ukiwa ni matoleo ya malimbuko yenu.