Walawi 19:26-37 Biblia Habari Njema (BHN)

26. “Msile nyama yoyote yenye damu. Msipige bao wala kufanya uchawi.

27. Nywele zenu msizikate pembeni wala kunyoa ndevu zenu.

28. Msijitie alama zozote mwilini mwenu kwa ajili ya kuomboleza au kujikatakata mwilini au kujichanja chale. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

29. “Usimchafue binti yako kwa kumfanya kahaba, nchi nzima isije ikaangukia katika ukahaba na hivyo kujaa uovu.

30. Mtazishika Sabato zangu na kupaheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

31. “Msiwaendee waaguzi wa mizimu wala wachawi ili kuwaomba wawaagulie na hivyo mkajitia najisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

32. “Uwapo mbele ya mzee ni lazima usimame ili kumpa heshima yake; nawe umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

33. “Kama kuna mgeni katika nchi yako usimtendee vibaya.

34. Huyo mgeni anayekaa nawe atakuwa kwako kama mwenyeji nawe utampenda kama unavyojipenda mwenyewe, kwa kuwa nawe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

35. “Usikose kamwe kuamua kwa haki kuhusu vipimo vya urefu, uzito na ujazo.

36. Ni lazima mtumie mizani halali, na vipimo vilivyo halali. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.

37. Ni lazima kuyashika na kuyatekeleza masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

Walawi 19