16. Kamwe usipitepite ukiwachongea watu wa jamaa yako. Usiyatie maisha ya jirani yako katika hatari ya kifo kwa maneno yako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
17. “Usimwekee kisasi ndugu yako moyoni mwako, bali upatane daima na jirani yako ili usije ukatenda dhambi.
18. Usijilipize kisasi au kuwa na kinyongo dhidi ya wazawa wa watu wako bali umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
19. “Yakupasa kuyashika masharti yangu. Usiiache mifugo yako ipandwe na wanyama wa aina nyingine. Shambani mwako usipande mbegu za aina mbili. Usivae vazi lililofumwa kwa aina mbili za nguo.
20. “Mwanamume akilala na mwanamke mtumwa ambaye ameposwa na mwanamume mwingine, lakini bado hajakombolewa wala kupewa uhuru, uchunguzi ufanywe. Lakini wasiuawe kwa sababu mwanamke huyo hakuwa bado huru.
21. Mwanamume huyo ataleta mbele ya hema la mkutano sadaka yake ya kondoo dume ya kuondoa hatia na kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu.
22. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa kutumia kondoo huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya dhambi aliyotenda; naye atasamehewa dhambi hiyo aliyotenda.
23. “Mtakapofika katika nchi ya Kanaani na kupanda aina zote za miti ya matunda, matunda hayo hamtayala; hamtaruhusiwa kuyala kwa muda wa miaka mitatu.
24. Mnamo mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa matakatifu, yatatolewa kuwa sadaka ya sifa, kwa Mwenyezi-Mungu.
25. Lakini matunda ya kuanzia mwaka wa tano hayo mnaweza kula, na mavuno yenu yataongezeka. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
26. “Msile nyama yoyote yenye damu. Msipige bao wala kufanya uchawi.
27. Nywele zenu msizikate pembeni wala kunyoa ndevu zenu.
28. Msijitie alama zozote mwilini mwenu kwa ajili ya kuomboleza au kujikatakata mwilini au kujichanja chale. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
29. “Usimchafue binti yako kwa kumfanya kahaba, nchi nzima isije ikaangukia katika ukahaba na hivyo kujaa uovu.
30. Mtazishika Sabato zangu na kupaheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
31. “Msiwaendee waaguzi wa mizimu wala wachawi ili kuwaomba wawaagulie na hivyo mkajitia najisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.