Walawi 18:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2. “Waambie watu wa Israeli hivi: Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

3. Kamwe msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Misri ambako mlikaa; wala msifanye kama wafanyavyo watu wa nchi ya Kanaani ambako nawapeleka. Kamwe msifuate mitindo yao.

4. Nyinyi mtafuata maagizo yangu na kuyashika masharti yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

5. Kwa hiyo, ili mtu apate kuyaokoa maisha, mnapaswa kuyashika masharti yangu na maagizo yangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

6. “Mtu yeyote wa Israeli haruhusiwi kumkaribia mtu wa jamaa yake wa karibu ili kulala naye. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

7. Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mama yako aliyekuzaa. Usimwaibishe; yeye ni mama yako.

8. Kamwe usimvunjie heshima baba yako kwa kulala na mmoja wa wake zake. Hao ni mama zako.

9. Kamwe usilale na dada yako, awe ni dada yako halisi au dada yako wa kambo.

Walawi 18