Walawi 14:37-49 Biblia Habari Njema (BHN)

37. Atauchunguza upele huo; kama upele huo umeonekana ukutani na umesababisha madoa ya rangi ya kijani kibichi au nyekundu na kuonekana kuwa yamepenya ndani ya kuta,

38. basi, kuhani atatoka nje mlangoni na kuifunga nyumba hiyo kwa muda wa siku saba.

39. Siku ya saba kuhani atarudi na kuiangalia tena nyumba hiyo. Ikiwa upele huo umeenea katika kuta za nyumba hiyo,

40. kuhani ataamuru mawe yaliyoko kwenye sehemu zenye upele yatolewe na kutupwa mahali najisi nje ya mji.

41. Lipu ya nyumba hiyo itabanduliwa na kifusi chake kutupwa mahali najisi nje ya mji.

42. Kisha watachukua mawe mapya na kujenga mahali walipobomoa; nao wataipiga nyumba hiyo lipu upya.

43. “Ikiwa upele huo utatokea tena baada ya kutoa mawe hayo na kukwangua lipu na kuipiga lipu upya,

44. yapasa kuhani aje kuichunguza. Ikiwa upele umeenea katika nyumba hiyo, basi huo ni upele wa kufisha; nyumba hiyo ni najisi.

45. Nyumba hiyo ni lazima ibomolewe na mawe yake, miti yake na lipu vipelekwe mahali najisi nje ya mji.

46. Zaidi ya hayo, yeyote atakayeingia ndani ya nyumba hiyo wakati itakapokuwa imefungwa, atakuwa najisi mpaka jioni.

47. Yeyote anayelala katika nyumba hiyo au kulia chakula ndani yake, lazima ayafue mavazi yake.

48. “Lakini ikiwa baada ya kuikagua nyumba hiyo, kuhani ataona kuwa upele haujaenea baada ya kupigwa lipu, basi, kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi kwani upele umekwisha.

49. Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili pamoja na kipande cha mwerezi, sufu nyekundu na tawi la husopo.

Walawi 14