13. “Ndege wote wafuatao ni najisi kwenu; hivyo msile: Tai, furukombe, kipungu,
14. mwewe, aina zote za kozi,
15. aina zote za kunguru,
16. mbuni, kirukanjia, dudumizi, aina zote za kipanga,
17. bundi, mnandi, bundi kubwa,
18. mumbi, mwari, mderi,
19. korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo.
20. “Wadudu wote wenye mabawa na waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu.
21. Lakini, baadhi ya wadudu wenye mabawa na wanakwenda kwa miguu minne ya kurukia ardhini mnaweza kula.
22. Hao ni: Kila aina ya nzige, kila aina ya senene, kila aina ya panzi na kila aina ya parare.
23. Lakini wadudu wengine wote wenye mabawa na miguu minne ni najisi kwenu.
24. “Kugusa wanyama fulanifulani humfanya mtu kuwa najisi; yeyote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni.
25. Mtu akichukua sehemu ya mizoga yake atakuwa najisi mpaka jioni, na mavazi yake ni lazima yafuliwe.
26. Mtu yeyote akigusa mnyama mwenye kwato zilizogawanyika lakini hacheui, mtu huyo atakuwa najisi.
27. Wanyama wote waendao kwa vitanga vyao ingawa wana miguu minne, ni najisi kwenu; na yeyote atakayegusa mzoga wa mnyama kama huyo atakuwa najisi mpaka jioni.
28. Mtu yeyote anayebeba mzoga atakuwa najisi, naye atasafisha mavazi yake. Hao ni najisi kwenu.
29. “Viumbe vifuatavyo ni najisi kwenu: Kicheche, panya, kila aina ya mjombakaka,
30. guruguru, kenge, mijusi, goromwe, na kinyonga.
31. Hao wote ni najisi kwenu na yeyote atakayegusa mizoga yao, atakuwa najisi mpaka jioni.
32. Ikiwa mzoga wa viumbe hao unakiangukia kitu chochote, kiwe ni kifaa cha mbao au vazi au ngozi au gunia au chombo chochote kitumiwacho kwa kusudi lolote lile, chombo hicho kitakuwa najisi mpaka jioni. Ili kukifanya kiwe safi ni lazima kukiosha kwa maji.