Waefeso 2:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.

4. Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,

5. hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa.

6. Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.

7. Ndivyo alivyopenda kuonesha kwa watu wa nyakati za baadaye ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu.

8. Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.

9. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

10. Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

11. Nyinyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine – mnaoitwa, “Wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) – kumbukeni mlivyokuwa zamani.

12. Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu katika yale maagano aliyoahidi Mungu. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani.

13. Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, nyinyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.

Waefeso 2