15. Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.
16. Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.
17. Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.
18. Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.
19. Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa majani ya mti wa husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha sheria na watu wote.
20. Mose alisema: “Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii.”
21. Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.
22. Naam, kadiri ya sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.
23. Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji tambiko iliyo bora zaidi.
24. Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.