1. Kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayotumainia; kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona.
2. Maana wazee wa kale walipata kibali cha Mungu kwa sababu ya imani yao.
3. Kwa imani sisi tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu; vitu vinavyoonekana kutoka vitu visivyoonekana.
4. Kwa imani Abeli alimtolea Mungu tambiko iliyokuwa bora kuliko ile ya Kaini. Kwa imani yake alikubaliwa na Mungu kuwa mwadilifu; Mungu mwenyewe alizikubali sadaka zake. Kwa imani yake ingawa alikufa, bado ananena.