4. Mataifa hayo yaliweka kambi nchini, yakawashambulia na kuharibu mazao yote nchini hadi mpakani mwa Gaza, wasiwaachie Waisraeli chochote, awe kondoo, ng'ombe au punda.
5. Adui waliozoea kuja kwa wingi kama nzige, pamoja na ng'ombe na ngamia wao na kufanya makao yao nchini Israeli, waliharibu nchi ya Israeli kwa vile walikuwa wengi mno wasiohesabika.
6. Waisraeli walidhoofishwa sana na Wamidiani hata wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie.
7. Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu awaondolee taabu walizopata kwa Wamidiani,
8. Mwenyezi-Mungu aliwapelekea nabii, naye akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Niliwatoa nchini Misri ambako mlikuwa watumwa,
9. nikawakomboa mikononi mwa Wamisri wote waliowakandamiza. Nikawafukuza watu mbele yenu na kuwapa nyinyi nchi yao.
10. Kisha nikawakumbusheni kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; na kwamba msiiheshimu miungu ya Waamori, ambao nchi yao mmeichukua, lakini hamkuisikiliza sauti yangu.’”
11. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akaenda, akaketi chini ya mwaloni wa Yoashi, Mwabiezeri, huko Ofra. Gideoni mwana wa Yoashi, alikuwa anapura ngano ndani ya shinikizo la kusindikia zabibu ili Wamidiani wasimwone.
12. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe, ewe shujaa.”