7. Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wake hao wanaume wa kabila la Benyamini waliosalia? Maana tulikwisha apa kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hatutawapa binti zetu wawe wake zao!”
8. Wakataka kujua kama kulikuwa na kikundi chochote cha makabila ya Israeli ambacho hakikuhudhuria mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Wakagundua kwamba hakuna mtu yeyote kutoka Yabesh-gileadi aliyekuja kwenye mkutano huo.
9. Waisraeli walipohesabiwa huko Mizpa hakuna mkazi yeyote wa Yabesh-gileadi aliyehudhuria.
10. Hivyo jumuiya ya Israeli ikapeleka watu wake 12,000 walio hodari kabisa na kuwaamuru: “Nendeni mkawaue wakazi wa Yabesh-gileadi; wanawake pamoja na watoto.
11. Mtawaua wanaume wote na wanawake wote wasio mabikira.”
12. Basi wakakuta miongoni mwa wakazi wa Yabesh-gileadi wasichana 400 ambao hawakuwa wamelala na mwanamume yeyote, wakawapeleka kambini huko Shilo katika nchi ya Kanaani.
13. Kisha jumuiya nzima ikawapelekea ujumbe wa amani watu wa kabila la Benyamini ambao walikuwa kwenye mwamba wa Rimoni.
14. Wanaume hao wa kabila la Benyamini wakawarudia hao wenzao wakati huohuo. Basi wakapewa wale wanawake ambao walikuwa wamesalimishwa huko Yabesh-gileadi. Lakini wanawake hao hawakuwatosha.
15. Waisraeli wakawaonea huruma watu wa kabila la Benyamini, maana Mwenyezi-Mungu alisababisha kuweko na mwanya katika Israeli.
16. Kisha wazee wa jumuiya nzima wakasema, “Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wanawake hao wanaume waliosalia kwa vile wanawake wote wa kabila la Benyamini waliangamia?
17. Lazima wanaume waliosalia wa kabila la Benyamini wapewe wanawake ili waendeleze kabila, na hivyo kusipotee kabila lolote katika Israeli.