Waamuzi 21:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Waisraeli walikuwa wameapa huko Mizpa kwamba hakuna hata mmoja wao ambaye angemwachia binti yake aolewe kwa watu wa kabila la Benyamini.

2. Basi, wakaenda mpaka Betheli wakakaa huko mbele ya Mungu hadi jioni. Wakapaza sauti na kulia kwa uchungu mwingi.

3. Wakasema “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limetukia hata tupungukiwe na kabila katika Israeli?”

4. Kesho yake watu waliamka mapema, wakajenga madhabahu, wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.

5. Kisha wakaulizana, “Je, miongoni mwa makabila yote ya Israeli kuna kikundi chochote ambacho hakikuhudhuria mkutano uliofanyika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Walikuwa wamefanya kiapo kwamba mtu yeyote ambaye hatahudhuria mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa ni lazima auawe.

6. Lakini Waisraeli wakawaonea huruma ndugu zao wa kabila la Benyamini, wakasema, “Leo kabila moja la Israeli limeangamia.

7. Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wake hao wanaume wa kabila la Benyamini waliosalia? Maana tulikwisha apa kwa jina la Mwenyezi-Mungu kuwa hatutawapa binti zetu wawe wake zao!”

Waamuzi 21