Waamuzi 16:13-17 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.”

14. Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia.” Samsoni akaamka kutoka usingizini akakingoa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo.

15. Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi.”

16. Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa,

17. hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.”

Waamuzi 16