1. Mungu akambariki Noa na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, muongezeke, mkaijaze nchi.
2. Wanyama wote, ndege wote wa angani, viumbe wote watambaao juu ya nchi na samaki wote wa baharini watakuwa na hofu na kuwaogopa nyinyi. Wote wamewekwa chini ya mamlaka yenu.
3. Wanyama wote hai watakuwa chakula chenu kama vile nilivyowapa mimea kuwa chakula chenu.
4. Lakini msile nyama yenye damu, kwani uhai uko katika damu.
5. Damu ya uhai wenu nitaidai; nitaidai kutoka kwa kila mnyama na binadamu. Atakayemuua binadamu mwenzake, nitamdai uhai wake.
6. Amwagaye damu ya binadamu,damu yake itamwagwa na binadamu;maana binadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu.
7. Nanyi zaeni, mkaongezeke;zaeni kwa wingi, mkaongezeke nchini.”
8. Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe,
9. “Ninaweka agano langu nanyi na wazawa wenu
10. na viumbe vyote hai: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wa porini, wote waliotoka katika safina pamoja nanyi.
11. Nathibitisha agano langu nanyi, kwamba, kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi.”