1. Kisha Yosefu alimwagiza msimamizi wa nyumba yake akisema, “Yajaze magunia ya watu hawa nafaka kiasi watakachoweza kuchukua. Halafu, weka fedha ya kila mmoja wao mdomoni mwa gunia lake.
2. Katika gunia la yule mdogo kabisa, kiweke kile kikombe changu cha fedha, pamoja na fedha yake.” Huyo msimamizi akafanya kama alivyoamriwa na Yosefu.
3. Kulipopambazuka wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao.
4. Walipokuwa wamesafiri mwendo mfupi tu kutoka mjini, Yosefu alimwambia msimamizi wa nyumba yake, “Haraka! Wafuate wale watu, na utakapowakuta, uwaulize, ‘Kwa nini mmelipa mema mliyotendewa kwa maovu? Kwa nini mmeiba kikombe cha bwana wangu ambacho
5. yeye hunywa nacho na kukitumia kupiga ramli? Mmekosa sana kwa kufanya hivyo!’”
6. Yule msimamizi alipowakuta akawaambia maneno haya.
7. Lakini wao wakamwuliza, “Bwana, una maana gani kutuambia maneno kama hayo? Sisi watumishi wako kamwe hatuwezi kufanya jambo kama hilo!
8. Kumbuka, bwana, fedha tuliyokuta katika midomo ya magunia yetu tuliirudisha kutoka katika nchi ya Kanaani. Itawezekanaje tena tuibe fedha au dhahabu nyumbani mwa bwana wako?
9. Basi, kama akipatikana mmoja wetu ana kikombe hicho, na auawe, na sisi wengine wote tutakuwa watumwa wako.”
10. Huyo msimamizi akasema, “Sawa; na iwe kama mlivyosema. Yeyote atakayepatikana na kikombe hicho, atakuwa mtumwa wangu, lakini wengine wote hamtakuwa na lawama.”
11. Basi, kila mmoja akashusha gunia lake chini haraka na kulifungua.