9. Mimi mwenyewe nitakuwa mdhamini wake. Wewe utanidai mimi. Nisipomrudisha ukamwona kwa macho yako mwenyewe, lawama na iwe juu yangu milele.
10. Kama tusingalikawia, tungalikuwa tumekwisha kwenda na kurudi mara mbili.”
11. Hapo Israeli, baba yao, akawaambia, “Haya! Kwa vile ni lazima iwe hivyo basi, fanyeni hivi: Chukueni katika mifuko yenu baadhi ya mazao bora ya nchi yetu, mkampelekee zawadi huyo mkuu. Mchukulieni mafuta kidogo ya mkwaju, asali kidogo, ubani, manemane, kungu na lozi.
12. Chukueni fedha mara mbili ya ile inayohitajika, kwa sababu ni lazima mrudishe fedha ile iliyowekwa midomoni mwa magunia yenu; pengine ilirudishwa kwa makosa.
13. Mchukueni pia ndugu yenu mwende kwa huyo mtu.
14. Mungu Mwenye Nguvu na awajalieni kupata huruma mbele ya mtu huyo, awaachieni yule ndugu yenu mwingine na Benyamini warudi pamoja nanyi. Kwa upande wangu, ikinipasa kufiwa na wanangu basi!”
15. Hapo, wakachukua zile zawadi, na fedha mara mbili ya zile za awali, wakaenda Misri pamoja na ndugu yao Benyamini. Walipowasili, wakaenda na kusimama mbele ya Yosefu.
16. Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wapeleke watu hawa nyumbani, umchinje mnyama mmoja na kumtengeneza vizuri, maana watu hawa watakula nami chakula cha mchana.”
17. Msimamizi huyo akafanya kama alivyoagizwa: Akawapeleka wale wageni nyumbani kwa Yosefu.
18. Walipoona wamepelekwa nyumbani kwa Yosefu, wakashikwa na hofu, wakasema wao kwa wao, “Tumeletwa huku kwa sababu ya ile fedha tuliyorudishiwa katika magunia yetu tulipokuja safari ya kwanza ili apate kisingizio cha kutushambulia ghafla na kutunyanganya punda wetu na kutufanya watumwa wake.”
19. Kwa hiyo wakamwendea yule msimamizi wa nyumba ya Yosefu wakaongea naye wakiwa mlangoni,
20. wakamwambia, “Samahani, bwana! Sisi tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.
21. Tulipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, tulifungua magunia yetu, tukashangaa kukuta fedha ya kila mmoja wetu mdomoni mwa gunia lake bila kuguswa. Sasa tumeirudisha fedha hiyo.
22. Tumeleta na fedha nyingine kununulia chakula. Hatujui ni nani aliyeweka fedha yetu katika magunia yetu.”