1. Kisha njaa ilizidi kuwa kali katika nchi ya Kanaani.
2. Baada ya kile chakula walichokuwa wamenunua kutoka Misri kumalizika, Yakobo akawaambia wanawe, “Nendeni tena Misri, mkatununulie chakula kidogo.”
3. Lakini Yuda akamwambia baba yake, “Yule mtu alituonya vikali, akisema, ‘Sitawapokea msipokuja na ndugu yenu mdogo.’
4. Kama utakubali ndugu yetu kwenda pamoja nasi, basi, tutakwenda kukununulia chakula.
5. Lakini iwapo hutakubali aende nasi, basi, hatutakwenda huko, kwani yule mtu alituambia waziwazi, ‘Hamtaniona msipokuja na ndugu yenu mdogo.’”
6. Israeli akasema, “Kwa nini mkanitia taabuni kwa kumwambia huyo mtu kwamba mnaye ndugu mwingine?”
7. Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa makini sana kuhusu mambo yetu na jamaa yetu akisema, ‘Je, baba yenu angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Hivyo tulimjibu kulingana na maswali yake. Tungaliwezaje kujua kwamba atatuambia, ‘Mleteni ndugu yenu?’”