Mwanzo 41:25-34 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto zako zote mbili tafsiri yake ni moja. Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni.

26. Ngombe wale saba wazuri ni miaka saba, na yale masuke saba mazuri pia ni miaka saba; ndoto hiyo tafsiri yake ni moja.

27. Wale ng'ombe saba waliokonda sana, ambao waliwafuata wale wanono, na yale masuke matupu saba, yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani, maana yake ni miaka saba ya njaa.

28. Kama nilivyokueleza, ee Farao, Mungu amekufunulia mambo atakayofanya hivi karibuni.

29. Kutakuwa na miaka saba ya shibe katika nchi nzima ya Misri.

30. Lakini baadaye itafuata miaka saba ya njaa, hata hiyo shibe isahaulike kabisa. Njaa hiyo itaiangamiza nchi hii.

31. Shibe hiyo itasahaulika kabisa kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.

32. Ndoto yako ilirudiwa mara mbili kwa mifano inayofanana kukuonesha kwamba Mungu ameamua, naye atatekeleza jambo hilo karibuni.

33. “Kwa hiyo yafaa sasa, ee Farao, umteue mtu mwenye ujuzi na hekima, umpe jukumu la kuiangalia nchi yote ya Misri.

34. Tena, ee Farao, uwateue wasimamizi kadhaa hapa nchini, uwaagize wakusanye sehemu ya tano ya mavuno yote ya Misri katika kipindi hiki cha miaka saba ya shibe.

Mwanzo 41