Mwanzo 29:20-33 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Basi, Yakobo akamtumikia Labani miaka saba kwa ajili ya Raheli, lakini kwake muda huo ulikuwa kama siku chache, kwa vile alivyompenda Raheli.

21. Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu.”

22. Basi, Labani akaandaa karamu na kuwaalika watu wote wa huko.

23. Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye.

24. (Labani akamtoa Zilpa, mjakazi wake, awe mtumishi wa Lea.)

25. Asubuhi, Yakobo akagundua ya kuwa ni Lea! Basi, akamwuliza Labani, “Umenitendea jambo gani? Je, si nilikutumikia kwa ajili ya Raheli? Mbona basi, umenidanganya?”

26. Labani akamjibu, “Nchini mwetu hatufanyi hivyo; si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya mkubwa.

27. Mtimizie Lea siku zake saba, nasi tutakupa Raheli kwa utumishi wa miaka saba mingine.”

28. Yakobo akakubali. Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake.

29. (Labani akamtoa Bilha, mjakazi wake, awe mtumishi wa Raheli).

30. Basi, Yakobo akalala na Raheli pia. Lakini Yakobo akampenda Raheli kuliko Lea; akamtumikia Labani miaka mingine saba.

31. Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Lea anachukiwa, akamjalia watoto; lakini Raheli alikuwa tasa.

32. Lea akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Reubeni, akisema, “Mwenyezi-Mungu ameyaona mateso yangu; bila shaka sasa mume wangu atanipenda.”

33. Lea akapata mimba tena, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Simeoni, akisema, “Mwenyezi-Mungu amenipa mtoto mwingine wa kiume kwa sababu amesikia jinsi ninavyochukiwa.”

Mwanzo 29