34. Yule mtu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu.
35. Mwenyezi-Mungu amembariki sana bwana wangu, naye amekuwa mtu maarufu. Amempa makundi ya kondoo na mifugo mingi, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda!
36. Sara, mke wa bwana wangu katika uzee wake, alimzalia bwana wangu mtoto; na bwana wangu amempa huyo mtoto mali yake yote.
37. Bwana wangu aliniapisha mimi akisema, ‘Hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ambao ninaishi katika nchi yao.
38. Bali utakwenda mpaka nchi yangu, kwa jamaa zangu, ili umtafutie mwanangu Isaka mke.’
39. Nami nikamwambia bwana wangu, ‘Huenda mwanamke huyo akakataa kufuatana nami kuja huku.’
40. Lakini yeye akasema, ‘Mwenyezi-Mungu aniongozaye maishani mwangu, atamtuma malaika wake aende pamoja nawe na kukufanikisha katika safari yako; nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka kwa jamaa yangu na nyumba ya baba yangu.
41. Kama utakapofika kwa jamaa zangu hawatakupa huyo msichana, basi, hutafungwa na kiapo changu.’
42. “Leo nilipofika kisimani nimeomba, ‘Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba nifaulu leo katika safari yangu na umfadhili Abrahamu bwana wangu.
43. Niko hapa kando ya kisima. Msichana atakayekuja kuteka maji ambaye nitamwomba anipatie maji kidogo ya kunywa kutoka mtungi wake,
44. naye akanipa na kuwatekea maji ngamia wangu, basi huyo na awe ndiye uliyemchagua kuwa mke wa mwana wa bwana wangu.’
45. “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, mara Rebeka alifika na mtungi wake wa maji begani, akateremka kisimani na kuteka maji. Nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ya kunywa.’
46. Naye akautua mtungi wake haraka kutoka begani mwake, akasema, ‘Haya, kunywa bwana wangu. Nitawatekea maji ngamia wako pia.’ Basi mimi nikanywa na ngamia wangu pia akawapa maji.
47. Ndipo nilipomwuliza, ‘Je, wewe ni binti wa nani?’ Akaniambia, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.’ Ndipo nilipompa pete na kumvisha bangili mikononi.
48. Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe.
49. Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.”
50. Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote.
51. Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.”
52. Mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno hayo, alimsujudia Mwenyezi-Mungu.