17. Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo.
18. Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.”
19. Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake.
20. Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana.
21. Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.
22. Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
23. Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.”
24. Abrahamu akasema, “Naapa.”
25. Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya.
26. Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.”
27. Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao.
28. Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba.
29. Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?”
30. Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.”
31. Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo.
32. Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti.
33. Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele.