Methali 24:15-30 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Usivizie kama mwovu kushambulia makao ya mtu mwema,wala usijaribu kuiharibu nyumba yake,

16. maana mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka,lakini mtu mwovu huangamizwa na janga.

17. Usishangilie kuanguka kwa adui yako;usifurahie moyoni mwako kujikwaa kwake,

18. maana Mwenyezi-Mungu aonaye hayo hatapendezwa;huenda akaacha kumwadhibu.

19. Usihangaike kwa sababu ya watenda mabaya,wala usiwaonee wivu watu waovu,

20. maana mwovu hatakuwa na mema baadaye;taa ya uhai wake itazimwa.

21. Mwanangu, umche Mwenyezi-Mungu na kumheshimu mfalme,wala usishirikiane na wale wasio na msimamo,

22. maana maangamizi yao huwapata ghafla.Hakuna ajuaye maafa watakayozusha.

23. Ifuatayo pia ni misemo ya wenye hekima:Kupendelea watu katika hukumu si vizuri.

24. Anayemwachilia mtu mwenye hatia,hulaaniwa na watu na kuchukiwa na mataifa.

25. Lakini wanaowaadhibu waovu watapata furaha,na baraka njema zitawajia.

26. Jibu lililo la haki,ni kama busu la rafiki.

27. Kwanza fanya kazi zako nje,tayarisha kila kitu shambani,kisha jenga nyumba yako.

28. Usishuhudie bure dhidi ya jirani yako,wala usiseme uongo juu yake.

29. Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda!Ni lazima nilipize kisasi!”

30. Nilipitia karibu na shamba la mvivu;shamba la mzabibu la mtu mpumbavu.

Methali 24