Methali 23:9-27 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Usiseme maneno yako mbele ya mpumbavu,maana atapuuza hekima ya maneno yako.

10. Usiondoe alama ya mpaka wa zamani,wala usiingilie mashamba ya yatima,

11. maana Mungu, Mkombozi, ni mwenye nguvu,naye ataitetea haki yao dhidi yako.

12. Tumia akili zako kufuata mafundisho;tumia masikio yako kusikiliza maarifa.

13. Usiache kumrudi mtoto;ukimchapa kiboko hatakufa.

14. Ukimtandika kiboko,utayaokoa maisha yake na kuzimu.

15. Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara,moyo wangu pia utakuwa wenye furaha.

16. Moyo wangu utashangilia,mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa.

17. Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi,ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote.

18. Hakika kuna kesho ya milele,na tumaini lako halitakuwa bure.

19. Sikia mwanangu, uwe na hekima;fikiria sana jinsi unavyoishi.

20. Usiwe mmoja wa walevi wa divai,wala walafi wenye kupenda nyama,

21. maana walevi na walafi wataishia kuwa maskini,anayetumia siku yake kusinzia atavaa matambara.

22. Msikilize baba yako aliyekuzaa,wala usimdharau mama yako akizeeka.

23. Nunua ukweli, wala usiuuze;nunua hekima, mafunzo na busara.

24. Baba wa mtoto mwadilifu atajaa furaha;anayemzaa mtoto mwenye hekima atamfurahia.

25. Wafurahishe baba na mama yako;mama aliyekuzaa na afurahi.

26. Mwanangu, nisikilize kwa makini,shikilia mwenendo wa maisha yangu.

27. Malaya ni shimo refu la kutega watu;mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba.

Methali 23