8. Ajipatiaye hekima anaipenda nafsi yake;anayezingatia busara atastawi.
9. Shahidi mwongo hatakosa kuadhibiwa;asemaye uongo ataangamia.
10. Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa,tena ni vibaya zaidi mtumwa kuwatawala wakuu.
11. Mwenye busara hakasiriki upesi;kusamehe makosa ni fahari kwake.
12. Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba,lakini wema wake ni kama umande juu ya majani.
13. Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake;na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha.
14. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake,lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
15. Uzembe ni kama usingizi mzito;mtu mvivu atateseka kwa njaa.
16. Anayeshika amri anasalimisha maisha yake;anayepuuza agizo atakufa.
17. Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu;Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema.