Methali 17:4-17 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya,mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu.

5. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake;anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa.

6. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao;watoto huwaonea fahari wazazi wao.

7. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu,sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi!

8. Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi;kila afanyacho hufanikiwa.

9. Anayesamehe makosa hujenga urafiki,lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki.

10. Onyo kwa mwenye busara lina maana,kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.

11. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu;mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake.

12. Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake,kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake.

13. Mwenye kulipiza mema kwa mabaya,mabaya hayataondoka nyumbani mwake.

14. Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa;achana na ugomvi kabla haujafurika.

15. Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatiayote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.

16. Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima,wakati yeye mwenyewe hana akili?

17. Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote,ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu.

Methali 17